Tuesday, July 7, 2015

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU - SEHEMU YA NNE

Karama ya unabii
I Wakorintho 12:4,10 ''Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii, na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha.
I Wakorintho 14:12; inasema ''.......takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa''.
Mambo ya msingi kuhusu huduma ya Nabii na karama ya unabii:-
1. kuna tofauti kati ya huduma ya nabii na karama ya unabii.
Efeso 4:11 ''Naye alitoa wengine kuwa Mitume; na wengine kuwa manabii....''. Hapa anazungumza habari ya nabii (ofisi) ya nabii. Huduma ni ofisi na karama ni vitendea kazi katika ofisi.


Kazi za nabii (kama huduma)


kufundisha mafundisho ya msingi / ya kuweka msingi wa kiroho ndani yako. Efeso 2:19-20 inasema, ''Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, ........mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni''. Hii haimaanishi kwamba kila nabii amepewa kufundisha.


Nabii pia anaweza kupewa kufanya kazi ya kubomoa na kuharibu kazi za shetani na kupanda pando la Mungu ndani ya mioyo ya watu, kama kuna mahali panahitajika kufanya hivyo. Tunaweza kusoma haya katika kitabu cha Yeremia 1:4,5,10; inasema '' .....kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa ............. Ili kung'oa na kubomoa na kuharibu na kuangamiza; ili kujenga na kupanda''.


Kazi nyingine ni kuonya. Tunaweza kuona haya katika kitabu cha Ezekieli 2:3-5; ''akaniambia mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israel, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi wao na baba zao wamekosa juu yangu.....''


Kazi nyingine ni mwonaji. I Samweli 9:9 ''(Hapo zamani katika Israel, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa mwonaji)''.


Kutabiri (kusema mambo yajayo). Yeremia 23:21; inasema ''mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.

Kazi ya karama ya unabii. (kama kitendea kazi):
Ni kujenga, kufariji, kutia moyo na kujirunza, pia huthibitisha kile ambacho Mungu amekwisha kusema na wewe. Katika kitabu cha I Wakorintho 14:3,4,24,25,31; tunasoma ''Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo. Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa. Lakini wote wakihutubu, kisha akaingia mtu asiyeamini, au mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote; siri za moyo wake huwa wazi, na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudi-fudi, na kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka. Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe''.

2. manabii wapo hata leo ila nafasi zao ni tofauti na za wale wa agano la kale.
Efeso 4:11,14; ''naye alitoa wengine kuwa mitume na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamisisha watakatifu; hata kazi ya huduma itendeke hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa Imani na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu............. Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja tukizifuata njia za udanganyifu''.
Pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume 13:1; tunasoma ''....... Palikuwako manabii na waalimu .....''. hii inaonyesha kuwa manabii wapo hata leo.
Tofauti iko hivi: kwamba manabii hapo zamani (katika agano la kale) walikuwa viongozi wakiongoza watu, yaani walipewa kuongoza watu, lakini katika agano jipya huduma ya nabii ipo ndani ya Kanisa na nabii hakupewa kuongoza kanisa- kila mmoja wakati huu amepewa Roho Mtakatifu ambaye anamwongoza. Hivyo nabii anayesema kwa mausia ya Mungu ni yule anayesema sawasawa na neno la Mungu.

Kanisa linajengwa juu ya misingi miwili ambayo ni:
a. Yesu Kristo
b. Mafundisho ya mitume na manabii ambao wanafundisha mafundisho ya msingi ambayo yanamfanya mtu awe mkristo. (foundation series). Ukisoma kitabu cha Waebrania 6:1; inasema ''kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundishao ya kwanza ya Kristo; tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na Imani kwa Mungu na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu na hukumu ya milele''.

Manabii wa sasa wanatofauti na akina Paulo na akina Petro ambapo hao wa zamani walipewa mafundisho ya msingi na hawa wa sasa wanapewa wito (hekima au special revelation) wanaposoma Biblia wanafungua siri za mafundisho ya msingi, ambayo akina Paulo walifundisha, na kutufunulia sisi.

Mambo ya msingi kuhusu huduma ya Nabii na karama ya Unabii, inaendelea........'
I Wakorintho 12:4,10
3. Karama ya Unabii (kinachosemwa na Nabii) lazima kipimwe.
Kwa nini kupima?


Si wote wametumwa na Mungu.
Ukisoma kitabu cha Yeremia 23:21,22; anasema ''mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao lakini walitabiri. Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya,.....''. Maana yake ni manabii wa kweli ila tatizo ni kwamba walienda pasipo kutumwa, hawakukaa barazani pa Mungu na kusikiliza kile ambacho Mungu alitaka kisemwe.


Kuna manabii wa uongo waliojiingiza katika makundi ya Mungu.
Ukisoma Mathayo 7:15; anasema ''Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.


Kuna manabii wa uongo ambao wanafanya kazi kwa kutumia Ishara na miujiza, ili kuwavuta watu wawafuate lakini Mungu hakuwatuma. Ukisoma Mathayo 24:24,25 ''kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa Ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini hata waliowateule. Tazama nimekwisha kuwaonya mbele''.


Kwa sababu ya matumizi yasiyo na utaratibu wa ki-Mungu juu ya huduma ya Nabii na karama ya unabii.
I Wakorintho 14:29,33,39,40; ''Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani, vile-vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu. Kwa ajili ya hayo ndugu, takeni sana kuhutubu wala msizuie kunena kwa lugha. Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na utaratibu''.


Ni agizo.
Ukisoma I Yohana 4:1; anasema '' Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani''. Pia katika kitabu cha 2 Petro 1:20,21; ''mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukutolewa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu''.

Unapimaje?
Katika kupima kwa ajili yako wewe kutoa karama ya Unabii au kwa kusikia kutoka mtu mwingine, jiulize maswali yafuatayo:-
a. Je roho inayokutumia kutoa unabii inakutawala au unaitawala? Ukisoma kitabu cha I Wakorintho 14:32,33 anasema ''Na roho za manabii huwatii manabii....'' Roho Mtakatifu hakuleta karama zake zikufanye mtumwa. Ukiona hali hii kaa kwenye maombi tena.
b. Je hayo yaliyosemwa kwa njia ya unabii ni sawasawa na neno? Ukisoma Warumi 12:6 inasema; ''......tutoe unabii kwa kadri ya imani''. Maana yake kwa kadri ya kiwango cha neno ulichonacho ndani yako. Pia kitabu cha Hesabu 22:18; inasema ''.....siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, alilosema ndani yangu Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza.
c. Je unapotumika katika unabii au kama nabii unajionaje ndani yako? Unaona kama hiyo karama ni kipimo cha kiroho kwamba uko mbali sana? Kitabu cha I Wakorintho 13:9 '' kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunafanya unabii kwa sehemu''. Maana yake hakuna mtu ambaye anajua kila kitu hivyo ni muhimu kuwa mnyenyekevu na kuwa tayari kujifunza kwa wengine.
Pia katika kitabu cha I Petro 4:9-10; inasema ''........ kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu''. Maana yake uwe tayari kupokea karama ambayo inatenda kazi ndani ya mtu mwingine. Vile-vile kitabu cha I Wakorintho 13:2; anasema '' tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, ..... kama sina upendo si kitu mimi''.
d. Je Kristo anainuliwa au la? Kitabu cha Kumbukumbu la torati 13:1-4. ''kukizuka katikati yako nabii au mwotaji wa ndoto... akisema, na tuifuate miungu mingine ya nabii yule ............ tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu, ........''. Kuna hatari pale ambapo karama zinafanya kazi halafu utukufu wanapewa watu badala ya kumwinua Yesu.
e. Je unabii / kilichosemwa na nabii au unabii ulioletwa kwako unakuweka huru au la? Maana palipo Roho wa Bwana hapo ndipo penye uhuru.
f. Je unabii huo unatimia au la? Ukisoma Kumbukumbu la Torati 18:20-22 anasema ''Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au takayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa...... atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana;.........''.
g. Je tabia za hao manabii zikoje? Ukisoma Mathayo 7:15-23; anasema '' ........mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.......... Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua..............''
Mara nyingi tunda huwa linachukua muda kutokea lakini baada ya muda huo litatokea tu.
h. Je huo ujumbe aliotoa nabii unajenga au unabomoa? Ukisoma I Wakorintho 14:3-5,31 '' Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo........... bali ahutubuye hulijenga kanisa ............ kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe''.

Karama ya unabii inavyofanya kazi


Kusema chini ya upako. 2 Petro 1:20-22 anasema '' ..........., wakongozwa na Roho Mtakatifu


Ujumbe unaoambatana na Matendo. Matendo ya mitume 21:9-14; inasema ''..... alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, hivyo ndivyo wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu nao watamtia katika mikono...........''.


Unabii mwingine unatimia kwa maombi. Yakobo 5:17-18; anasema '' Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia pamoja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinye na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua nayo nchi ikazaa matunda yake''.

No comments:

Post a Comment