Mchungaji mmoja rafiki yangu aliniambia asilimia hamsini mpaka sabini ya changamoto au matatizo anayoshughulika nayo mara kwa mara katika kanisa lake ni ya wanandoa. Kwa lugha nyepesi asilimia 50 – 70 ni matatizo yatokanayo au yanayohusiana na ndoa. Binafsi pia kwa upande wangu kupitia nafasi yangu katika mwili wa Kristo, email za wasomaji ninazopata na pia baadhi ya semina za ndoa ambazo nimefanya kuhusu eneo hili nimegundua kwa hakika ndoa nyingi za wana wa Mungu zina shida na wao hawajajua kwamba vita hii inatoka kwa Shetani, maana anajua ndoa zikitengamaa ni faida kwa ufalme wa Mungu na ni uharibifu kwenye ufalme wake wa giza. Naam anapigana usiku na mchana ili kuhakikisha ndoa hazitengamai kwa kuleta fujo za kila aina.
Kila siku katika ndoa kuna changamoto zinazaliwa mpaka imefika mahala baadhi ya wanandoa wanawaza kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Kwa hakika laiti Biblia ingetoa mwanya kwa wanandoa kuachana basi kuna baadhi ya wanandoa wangehakikisha wanaitumia hiyo nafasi vizuri kwa kuwa ndoa zimegeuka ndoano. Matarajio ambayo kila mmoja alikuwa nayo kwenye ndoa anaona hayatimii. Kinachosumbua watu wengi ni kwamba kabla hawajaonana hawakujua nini kinakuja kupitia ndoa, hawakuweza kuona uhalisia wa maisha ya ndoa utakuwaje? Bali kila mmoja alikuwa na mtazamo/fikra na matarajio yake binafsi juu ya ndoa yake.
Naam zipo sababu nyingi sana zinazopelekea matatizo au changamoto kwa wanandoa. Katika somo hili nitaandika zaidi zile zinazotokana na upinzani kutoka kwa Shetani ili kuathiri kusudi la Mungu. Lengo la ujumbe huu ni kukufundisha wewe mama (Mwanandoa) namna ya kuzitumia ‘nafasi’ ambazo Mungu amekupa Kibiblia ili kuiponya ndoa yako au kubadilisha hali ya sasa ya ndoa yako endapo unaona si ile ambayo Mungu amekusudia.
Kwa nini Mwanamke?
Pengine utaniuliza kwa nini mwanamke ndiye awajibike katika kuponya au kubadilisha maisha ya ndoa yake? Binafsi katika kuisoma Biblia nimegundua kwamba kwa kuzingatia nafasi ambazo mwanamke amepewa kibiblia ni ishara ya kwamba kwa habari ya ndoa, Mwanamke ana nafasi kubwa ya kuijenga au kuibomoa ndoa yake na hivyo nyumba yake kwa ujumla. Mara kwa mara Mungu ananifundisha masuala ya wanawake, suala la wanawake kuwa kwenye ‘nafasi zao’ husisitizwa sana.
Kwa nini nafasi?
Sijui kama unafahamu maana ya nafasi ambayo Mungu anampa mtu katika ulimwengu wa roho. Hizi ni nafasi ambazo Mungu amekupa wewe mawanamke katika ulimwengu wa roho ili uzitumie kufanikisha kusudi lake kupitia ndoa yako. Nafasi (position) ni eneo ambalo mtu anapaswa kuwepo kwa kuhusianisha na vitu au watu wengine, naam ni wadhifa ambao mtu anakuwa nao kwa kuhusianisha na mtu au watu wengine.
Kwa hiyo hizi ni nafasi ambazo Mungu amempa mwanamke zikihusiana na mwanaume katika kilitumika kusudi la Mungu hapa duniani. Mwanamke anapokuwa amesimama katika nafasi zake ndipo anapoweza kuruhusu mawazo ya Mungu kupitia ndoa yake kutimia naam ndivyo anavyoweza kuzuia mawazo ya Iblisi kupitia ndoa yake yasitimie. Naam nafasi ya mwanamke katika ndoa ndiyo inayoamua uzima au mauti ya ndoa yake, nafasi ndiyo inayopelekea kufanikiwa au kufeli kwa ndoa yake, nafasi ya mwanamke katika ndoa ndio inayoamua nini kingie au kitoke kwenye ndoa.
Katika kusoma kwangu Biblia nimegundua kwamba Mungu amempa nafasi zifuatazo mwanamke;
- Mwanamke kama ‘msaidizi’ wa mumewe
- Mwanamke kama ‘mlinzi’ wa mwanaume
- Mwanamke kama ‘mjenzi’ wa nyumba yake
- Mwanamke kama ‘mshauri’ wa mumewe
- Mwanamke kama ‘mleta kibali’ kwa mumewe
Somo litaendelea, maombi yako ni muhimu sana.
No comments:
Post a Comment