Na Sarah Pelaji
Tunapofanya kumbukumbu ya miaka 25 tangu alipotutembelea Mtakatifu Yohane Paulo II (Papa) mwaka 1990, ni vyema tukarejea maneno ya hekima aliyotuletea kama zawadi sisi watoto wa Tanzania.
Ni maneno ambayo ni hai katika maisha yetu ya kila siku hasa pale tunapoelemewa na mizigo ya ulimwengu huu, dhambi zetu na matatizo mbalimbali ya kiroho na kimwili ambayo yanawakatisha wengi wetu tamaa na kuona zawadi ya maisha haina maana tena.
Basi tufarijiwe na maneno haya ya Mtakatifu Yohane Paulo II (Papa) aliyoyatoa katika Kanisa Kuu la Mtaatifu Yosefu Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
“Ndugu zangu, Amani ya Bwana iwe nanyi.
Nimekuwa nikiisubiri kwa hamu sana nafasi hii ya kuitembelea Tanzania, kukutana na Wakatoliki wake na watu wote wenye nia njema katika hali ya udugu na amani. Nimekuja kama shahidi kwa Kristo, kuwadhibitishieni ninyi katika injili ya wokovu mlioipata na mnayozingatia kwa kuwa sasa nimeshawasili Dar es salaam, “ Bandari ya amani”, mawazo yangu yanageukia maneno ya Kristo kwa mitume wake muda mfupi kabla ya mateso. “ Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu wala msiwe na uoga “ ( Yn 14:27 ).
Mwanzoni mwa ziara yangu ya Kiaskofu, sala yangu ya nguvu ni kwamba kila mmoja wenu asikie ndani kabisa moyoni mwake na katika familia, Parokia ya jumuiya zenu zawadi ya Kristo ya amani.
Ningependa kuanza kwa kumshukuru Kardinali Laurean Rugambwa kwa maneno yake mazuri ya makaribisho. Kwa karibu nusu karne amejitolea kwa moyo wote kulifanyia kazi Kanisa kama Padri, Askofu Mkuu mwandamizi Polycarp Pengo, ninyi nyote, katika kumwomba Mungu amjalie Mwadhama miaka mingi ya furaha kwenye kazi yake ya kumtumikia Bwana.
Hivi punde Kardinali amezungumzia umuhimu wa kutangaza “ Habari njema za Yesu Kristo nchini Tanzania, kati kati ya matatizo ya kijamii na mmomonyoko wa maadili ya kiroho na kilimwengu hasa kwa kuwa yanaathiri sana familia. Nguvu zangu wapendwa ni Kristo pekee anayeweza kuponya majeraha ya uovu na dhambi; ni kristo pekee anayeweza kuondoa kukata tamaa kunakoisumbua mioyo mingi, kwasababu ni Kristo pekee anayeweza kumpatanisha mwenye dhambi na Mungu pamoja na watu wengine kupitia msalaba na ufufuko. Zawadi ya Mungu ya upatanisho katika Kristo ni chanzo cha ile amani tunayoitamani sana, “ Amani niwapayo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo” ( Yn 14:27 ).
Zaidi ya karne moja iliyopia Wamisionari walileta zawadi ya Kristo ya upatanisho na amani kwa watu wa nchi hii. Kuanzia mwaka 1887 Shirika la Benedict la Mtakatifu Otilia la huko Ujerumani lilikabidhiwa kile kilichojulikana kama Vicarite Apostolic ambalo sasa ni Jimbo Kuu la Dar es salaam. Mabaki ya Askofu Cassian Spiess na wale waliouwawa pamoja naye kwenye miaka ya mwanzoni mwa karne hii – yaliyozikwa katika Kanisa Kuu hili – yanasaidia kuthibitisha kuwa zawadi ya Kristo ya amani si ya dunia hii bali ni matunda ya kuungana nae katika fumbo la kifo na ufufuko wake.
Ninyi mlio watoto wa kiroho wa Wamisionari mmepata fursa njema ya kuona Kanisa changa lenye msimamo likiibuka kutokana na dhabihu za Wamisionari hao. Ni Kanisa lenye ushuhuda wa habari njema za wokovu katikati ya furaha na maadili ya Watanzania, na kadhalika na majonzi na majaribu yao, na shida na mashaka yao. Mkiwa Waumini wa Kanisa lenye safari ngumu, mnasonga mbele mkisadiki kuwa “ imani huleta mwangaza kwa vitu vyote na hutambulisha utimilifu kamili uliotayarishwa na Mung kwaajili ya binadamu” ( Gaudium et Spes, 11 ).
Ingawa utimilifu huu unapatikana katika ukamilifu wa maisha ya milele tu, hata hivyo unamsukuma binadamu kuyakabili matatizo na changamoto kila anapokutana nayo kama iwapasavyo kufanya mitume wa Kristo katika mfano wa kusisimua Roho Mtakatifu Paulo, ‘ basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguuni utayari tupatao kwa injili ya amani zaidi ya yote mkiitwa ngao ya imani, ambayo kwahiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule movu “ ( Efe 6:14-16).
Ndio, ndugu zangu wapendwa ninyi ni mashuhuda wa “ injili ya imani” nchini Tanzania. Mnaishi nayo kila siku katika familia zenu, katika jumuiya zenu, kazini mwenu, na zaidi ya hapo ndani ya Kanisa, ambalo ni “ alama na ala ya ufungamano na mungu nay a umoja wa binadamu wote” ( Lumen Gentium 1 ). Ufungamano na mungu, umoja baina ya wanadamu ; hii ndiyo imani ya ufalme ujao ambayo inakisiwa hata sasa katika maisha yenu ya Kikristo.
Jioni hii tumekusanyika katika Kanisa Kuu ambalo linatukumbusha upendo mkubwa wa Wamisionari Wabenediktini kwa Kristo na watu wa nchi hii, upendo uliofikia hadi hatua ya kumwaga damu kwaajili yake. Kanisa hili lilitolewa kwa Mtakatifu Yosefu, mumewe Bikira Maria, wakiwa na imani ya fadhili zake kwa niaba ya jitihada zao za kimisionari.
Fadhila hizi yafaa daima zitumiwe na Kanisa kama kichocheo cha kuzidisha harakati za uenezaji wa injili. Mtakatifu Yosefu awe mwalimu wa kipekee kwenu nyote katika huduma hii ya kazi ya wokovu kazi ambayo ni jukumu la kila muumini wa jumuiya ya Kristo ( mawaidha ya kitume, Rwdemptoris Custos, 29, 32 ).
Matumaini yangu ni kuwa Yosefu, “ mtu wa haki “ ( Mt 1:19 ), atawaombea kwa Mungu – Maaskofu, Mapandri, Watawa na Walei wa Kanisa la Tanzania ili kwamba “ amani ya kristo itawale mioyoni mwenu “ ( Bandari ya amani ) ya kweli sasa na daima.
Mungu awabariki na kuwalinda. Amina.
No comments:
Post a Comment