TUJIFUNZE KATIKA MLANGO NA MUNGU ATAWABARIKI SANA.
1 Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi.
2 Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu,
3 akiyafunua na kuwaeleza ya
kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba,
Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo.
4 Wengine miongoni mwao
wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu,
wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache.
5 Na Wayahudi wakaona wivu,
wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema,
nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa
nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji;
6 na walipowakosa, wakamkokota
Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele,
wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,
7 na Yasoni amewakaribisha; na
hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema
na kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu.
8 Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo.
9 Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao.
10 Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.
11 Watu hawa walikuwa waungwana
kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu
wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo
ndivyo yalivyo.
12 Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache.
13 Lakini Wayahudi wa
Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na
Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawachafua na
kuwafadhaisha makutano.
14 Mara hiyo wale ndugu wakampeleka Paulo aende zake mpaka pwani; bali Sila na Timotheo wakasalia huko.
15 Lakini wale waliomsindikiza
Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea
Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao.
16 Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake.
17 Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku.
18 Na baadhi ya Waepikureo na
Wastoiko, wenye ujuzi, wakakutana naye. Wengine wakasema, Mpuzi huyu
anataka kusema nini? Wengine walisema, Anaonekana kuwa mtangaza habari
za miungu migeni, kwa maana alikuwa akihubiri habari za Yesu na ufufuo.
19 Wakamshika, wakamchukua Areopago, wakisema, Je! Twaweza kujua maana ya elimu hii mpya unayoinena?
20 Kwa maana unaleta mambo mageni masikioni mwetu, tutapenda kujua, basi, maana ya mambo haya.
21 Kwa maana Waathene na wageni
waliokaa huko walikuwa hawana nafasi kwa neno lo lote ila kutoa habari
na kusikiliza habari za jambo jipya.
22 Paulo akasimama katikati ya
Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa
ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.
23 Kwa sababu nilipokuwa
nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu
iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi
nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.
24 Mungu aliyeufanya ulimwengu
na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi,
hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono;
25 wala hatumikiwi kwa mikono
ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye
anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.
26 Naye alifanya kila taifa la
wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha
kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;
27 ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.
28 Kwa maana ndani yake yeye
tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga
mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.
29 Basi, kwa kuwa sisi tu wazao
wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha
au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.
30 Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.
31 Kwa maana ameweka siku
atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye
amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.
32 Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo.
33 Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha.
34 Baadhi ya watu wakashikamana
naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke
mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao.